16 Julai 2026 - 12:35
Kiongozi wa Wanazuoni wa Imamiyya Pakistan: Vikwazo kwa Mazuwwari wa Arubaini ni Sehemu ya Mardi wa Kuwadhoofisha Mashia

Kiongozi wa Baraza la Wanazuoni wa Imamiyya Pakistan, Hujjatul Islam Dkt. Sayyid Shafaqat Hussein Shirazi, amesema vikwazo vinavyowakabili mahujaji wa Pakistan kuelekea Arubaini si suala la kiusalama pekee, bali ni sehemu ya mpango wa kudhoofisha uhusiano wa wafuasi wa Ahlul-Bayt (as) na Iran, Iraq pamoja na utamaduni wa A'shura.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Kiongozi wa Baraza la Wanazuoni wa Imamiyya Pakistan na Mkuu wa Masuala ya Nje wa Majlis-e-Wahdat-e-Muslimeen Pakistan, Hujjatul Islam Dkt. Sayyid Shafaqat Hussein Shirazi, amesema kuwa vikwazo vinavyowekwa dhidi ya mahujaji (mazuwwari) wa Pakistan wanaokusudia kushiriki matembezi makubwa ya Arubaini ni mwendelezo wa mradi wa kuwadhoofisha wafuasi wa Madhehebu ya Ahlul-Bayt (as) katika eneo.
 
Akizungumza na ABNA, Dkt. Shirazi alisema kuwa kuzuiwa kwa mahujaji kutumia njia za ardhini kuelekea Iraq kupitia Iran hakupaswi kutazamwa kama suala la kiusalama pekee, bali ni sehemu ya juhudi za kuvunja uhusiano wa kidini, kitamaduni na kijamii kati ya Waislamu wa Pakistan, Iran na Iraq.
 
Alieleza kuwa kuna juhudi za kupunguza athari za ujumbe wa A'shura na utamaduni wa kujitolea kwa ajili ya haki, huku akidai kuwa baadhi ya mataifa yenye ushawishi yanataka kueneza kile alichokiita "Uislamu wa Kimarekani" badala ya Uislamu halisi unaotokana na mafundisho ya Mtume Muhammad (saww) na Ahlul-Bayt (as).
 
Aidha, alisema kuwa asilimia 70 hadi 80 ya Mazuwwari wa Pakistan husafiri kwa njia ya ardhini kutokana na gharama nafuu, hivyo kufungwa kwa njia hizo kunawanyima mamia ya maelfu ya waumini fursa ya kushiriki ziara ya Arubaini na kuzuru maeneo matakatifu nchini Iraq na Iran.
 
Dkt. Shirazi alikumbusha kuwa mwaka uliopita, kufungwa kwa ghafla kwa njia za usafiri kabla ya Arubaini kulisababisha hasara kubwa za kifedha kwa mahujaji waliokuwa tayari wamelipia visa, tiketi, hoteli na usafiri.
 
Ametoa wito kwa serikali za Pakistan, Iran na Iraq kuongeza ushirikiano, kufungua tena njia za ardhini na kurahisisha taratibu za safari ili kuwawezesha mahujaji kutekeleza ibada hiyo muhimu kwa usalama.
 
Katika hitimisho lake, Dkt. Shirazi alisema kuwa suluhisho la changamoto zinazowakabili mahujaji wa Pakistan linahitaji zaidi utashi wa kisiasa kuliko jambo lingine lolote, akisisitiza kuwa mamlaka zikiamua kulinda usalama wa raia na mahujaji, tatizo hilo linaweza kutatuliwa kwa haraka.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha